Mwanasiasa na Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya ameiambia Dar24 kuwa yeye ni muumini wa Siasa za ushindani, siasa za hoja na siasa za kweli huku akitoa shukrani zake kwa Chama cha Mapinduzi – CCM, kwa kumtoa mbali, kumtengeneza, kumpika na kwamba bado hajabadilika kwani yeye ni mjenzi wa hoja zenye mashiko.
Bulaya aliyasema hayo hivi karibuni, katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Dar24 jijini Dodoma na kuongeza kuwa pia anapenda kuwa mwenyewe, ili aweze kujitegemea kwa maslahi mapana ya nchi na alihama chama kutokana na aina za Siasa alizozihitaji ambazo anahisi zina mchango mkubwa wa ustawi wa Taifa.
Amesema, “mimi nitoe shukrani zangu kwa CCM, kwa kunitoa mbali, kunitengeneza, kunipika na hata nikiwa Mbunge wa Vijana wa CCM, Ester Bulaya hajabadilika ni muumini wa kujenga hoja za maslahi ya nchi, lakini kwa aina ya siasa wanazozitaka niliona nitafurahia zaidi nikiwa upinzani na chama ambacho nilikiona ni sahihi kwangu ni CHADEMA.”
Kuhusu Bunge la Tanzania na siasa za ushindani, Bulaya amesema anakumbuka hali ilivyokuwa mwanzo, kwani kwa sasa ni kama ushindani umepungua kwani kwa zaidi ya asilimia 96 mpaka 7 Wabunge wote ni wa Chama cha Mapinduzi na hali hiyo haina ladha kwani hata kwa idadi yao ndogo Bungeni bado wananyimwa nafasi ya kuchangia mijadala.
“Tupo 19 tu wanatunyima tusichangie, tupo 19 tu wanaogopa hata tusiende kwenye hatua ya shilingi, yaani hakuna ladha tofauti na kipindi kile ambapo tulikuwa Wabunge karibia au 100, je tungekuwa kama wale wengi ingekuwaje? ni kama wanakimbia kivuli chao kwa kutuhofia siye wachache,” amesema Bulaya.
Hata hivyo, amesema endapo itatokea kila Mbunge akatambua wajibu wake na kile kilichompeleka Bungeni, itasaidia kuisukuma Serikali katika utendaji kwani Wananchi pia wanaangalia uwezo wa Viongozi wao katika kuwawakilisha na kuwasemea changamoto zao, ili ziweze kutatuliwa.