Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema Sergio Aguero alidanganya katika tukio lililopelekea kiungo Marouane Fellaini kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa mshambuliaji huyo.
Fellaini, 29, alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 84 sekunde chache baada ya kuonyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu raia huyo wa Argentina.
Mchezo huo wa ‘derby’ ya jiji la Manchester uliofanyika kwenye uwanja wa Etihad ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
“Sikuona vizuri tukio lakini naweza kuhisi, kadi nyekundu ilikuwa nyepesi kwa uzoefu wangu mdogo. Mchezaji wa Kiargentina alikuwa bora katika tukio hili,” alisema Mourinho.
Akijibu swali kama raia huyo wa Ubelgiji alifanya ‘ujinga’ kwa tukio hilo Mourinho aliongeza: “Marouane alisema ilikuwa ni kadi nyekundu kwa kuwa yeye ni Marouane.
Mwamuzi (Martin Atkinson) aliniambia kwa maoni yake ilikuwa ni kadi nyekundu, lakini nilimuona Aguero akianguka hakuvunjika pua wala kichwa sura yake ilikuwa nzuri kama kawaida. Sina uhakika.
“Kama Sergio asingeanguka chini isingekuwa kadi nyekundu, lakini Marouane alimpa nafasi ya kufanya hivyo. Sijui lakini ninachofahamu tulicheza dakika 15 tukiwa 10 na vijana walipambana kupata pointi.”
Felliani alitolewa nje kwa kadi nyekundu mara tatu tangu alipojiunga na United akitokea Everton kwa ada ya pauni 27.5 milioni Septemba 2013.
Alitolewa nje kwenye mchezo wa ligi uliomalizika kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Hull City Mei 24, 2015 na ule wa ligi ya mabingwa dhidi ya Real Sociedad Novemba 2013.
Fellaini pia alitolewa nje katika mchezo wa ligi ulioisha kwa sare ya bao 1-1 kati ya Everton na Bolton Novemba 2010.