Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wamefanikisha mpango wa kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa pembeni kutoka Ufaransa Kingsley Coman, aliyekuwa klabuni hapo kwa mkopo wa misimu miwili akitokea Juventus ya Italia.

Coman mwenye umri wa miaka 20, amesaini mkataba wa miaka mitatu na ataitumikia miamba hiyo ya Bundesliga mpaka mwaka 2020. Dau la Euro Milioni 21 linatajwa kutumika kwenye usajili wa kinda huyo.

Coman alijiunga na Bayern Munich mwaka 2015 akitokea Juventus kwa uhamisho wa mkopo wa misimu miwili uliokuwa na kipengele cha kusajiliwa moja kwa moja kabla ya Mei 2017.

Mpaka sasa Coman amefanikiwa kuichezea Bayern Munich michezo 58 na kuifungia mabao manane.

Kabla ya kutua Juventus mwaka 2014 na kisha Bayern Munich mwaka 2015, safari ya kisoka ya Coman ilianzia katika klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa ambapo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi pale alipokichezea kwa mara ya kwanza kikosi cha wakubwa cha miamba hiyo akiwa na umri wa miaka 16 na miezi minane na siku nne.

Sergio Aguero Amchefua Jose Mourinho
Twiga Stars Kutajwa Mwezi Ujao