Kocha mkuu wa timu za taifa za wanawake Sebastian Nkoma anatarajia kutangaza kikosi cha Twiga Stars, ambacho kitaingia kambini mapema mwezi ujao jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuajiandaa na michezo ya kufuzu fainali za Afrika za 2018 zitakazochezwa Ghana.

Mwenyekiti wa soka la wanawake nchini (TWFA), Amina Karuma amesema, Kocha Nkoma atatangaza kikosi chake, kwa mujibu wa tathmini aliyoifanya wakati wa michuano ya ligi kuu ya wanawake, ambayo ilichezwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania msimu wa 2016/17.

“Tunataka timu iingie kambini mapema iwezekanovyo ili kumpa nafasi kocha mkuu kuendesha Programu zake kwa nafasi, na kambi itakua hapa katika hosteli za TFF jijini Dar es salaam.”

“Tunaamini kwa kipindi ambacho kocha atakua na wachezaji kambini ataweza kuwachuja wachezaji hadi kufikia idadi tunayoikusudia kwa ajili ya kuwa na timu nzuri ya taifa ya wanawake itakayoingia kwenye harakati za kusaka nafasi ya kucheza fainali za Afrika za mwaka 2018.” Amesema Karuma.

Katika hatua nyingine Bi. Karuma amezungumzia hatma ya kocha Nasra Juma ambaye kwa kipindi kirefu amekua haonekani katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania (Twiga Stars).

“Suala na Nasra litatolewa ufafanuzi na katibu mkuu wa TFF, lakini kwa uchache bado tupo naye, na amekua msaada mkubwa katika maendeleo ya soka la wanawake katika pande zote mbili za muungano.”

Kocha Nasra Juma aliondoka Dar es salaam mwishoni mwaka jana na kurejea kisiwani Ungunja (Zanzibar) kwa ajili ya kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya visiwa hivyo, ambayo ilishiriki fainali za Afrika mashariki na kati zilizofanyika nchini Uganda na Tanzania bara ikaibuka na mabingwa.

Kingsley Coman Atimiza Ndoto Zake
Video: Coyo MC na Maajabu Aliyoyaona Jukwaani, awataja Fid Q na Young Killer