Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Machano Othman Said juu ya lini Serikali itaweka utaratibu wa kupunguza riba ya mikopo walau kufikia asilimia 10 – 12 badala ya sasa ambayo ni asilimia 17 – 20.
“Mabadiliko ya Sekta ya Fedha ya mwaka 1991 yalipelekea Serikali kujitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki nchini ili kuruhusu mfumo wa soko huria, hususan nguvu ya soko kuamua viwango vya riba za mikopo, riba za amana na gharama nyingine za huduma za kibenki,” amesema Dkt. Ashatu Kijaji.
Amesema kuwa viwango vya riba za mikopo na riba za amana pamoja na riba za mikopo kati ya benki na benki hupangwa kwa kuzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, gharama za uendeshaji, riba za dhamana za Serikali, sifa za mkopaji na hatari ya mkopaji kutolipa mkopo pamoja na kasi ya mfumuko wa bei.
Aidha Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza.
Vile vile amesema kuwa kiwango cha hatari ya kutolipa mkopo ni miongoni mwa vigezo vinavyotumiwa na mabenki katika kupanga viwango vya riba za mikopo, ambapo kwa sehemu kubwa gharama za riba za mikopo hutegemea zaidi gharama za upatikanaji wa fedha pamoja na gharama za uendeshaji.