Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye jumla ya Shilingi 1,867,896,520 kwa vikundi vya vijana 309 katika Halmashauri 94.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde, Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge  wa Viti Maalum Zainab Katimba alipotaka kujua idadi ya vijana walionufaika  kupitia mfuko huo na namna ambavyo mikopo hiyo imebadilisha maisha yao.

“Lengo la kuanzishwa kwa mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini (Tanzania Bara) kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali,” amesema Mavunde.

Aidha, amesema kuwa fedha za mikopo zitokanazo na Mfuko huo umekuwa msingi mzuri katika kuwaandaa vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine na hata kukuza vipato vyao.

Mavunde ametaja shughuli ambazo vijana hao wamekuwa wakishiriki mara wanapopata mikopo hiyo kuwa ni uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, kilimo, ufugaji pamoja usindikaji wa mazao.

Aidha amesema kuwa shughuli hizo zimewafanya vijana kuachana na utegemezi na badala yake kutumia muda wao mwingi katika kuzalisha na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Nchi.

Vile vile amesema kwamba, vipo vikundi ambavyo kupitia mfuko huo vimekuwa kielelezo cha dhati katika kubadili mtizamo wa  vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi kujiajiri wenyewe na kukuza vipato vyao.

Hata hivyo amevitaja vikundi hivyo kuwa ni kikundi cha Thyroid Group kutoka Halmashauri ya Chunya ambacho kinasambaza Taa za Solar Vijijini, kikundi cha Miranaco Group ambacho kinamiliki duka kubwa la dawa za Binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi, kikundi cha Maswa Family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu Milk kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.

 

Serikali kuboresha fursa ajira za vijana nchini
Serikali haina mamlaka ya kuweka ukomo wa riba