Serikali Nchini, itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wenye Viwanda, Wafanyabiashara na Wawekezaji, kushiriki katika ukuzaji wa uchumi hususan kwenye Sekta ya Viwanda.
Hayo yamebainishwa hii leo Oktoba 15, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango kwenye Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Mtambo Mpya wa Mabati ya Rangi, wa kampuni ya ALAF jijini Dar es Salaam.
Amesema, tukio hilo ni sehemu ya matunda ya juhudi kubwa zinazofanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji na pia kwa maono yake ya kuiamini Sekta Binafsi katika kujenga uchumi imara wa nchi.
“Napenda kuwaahidi kwamba, wenye viwanda, wafanyabiashara na wawekezaji, Serikali itawapa ushirikiano. Kwa upande wenu, mnao wajibu wa kuzingatia uendelevu wa ubora na tija kulingana na viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa katika shughuli za uzalishaji hatimae kunufaika zaidi na fursa za masoko zilizopo na zinazoendelea kujitokeza,’’ ameeleza Dkt. Biteko
Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa ALAF Limited, Ashish Mistry, Bodi na Menejimenti ya kiwanda cha ALAF kwa kuamua kujenga mtambo huo wa kwanza nchini na wa kisasa utakaotumika kutengeneza mabati ya rangi nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kuzinduliwa kwa mtambo huo kunatoa fursa mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huo ikiwemo nafasi za ajira zitakazotolewa na kiwanda hicho kwa Watanzania.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania – TBS, Dkt. Athuman Angenya amesema kuwa kiwanda hicho kimeendelea kutengeneza bidhaa zenye ubora nchini jambo linalofanya wafanye vizuri katika soko.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania – TIC, Dkt. Bilinith Mahenge amesema kuwa kituo hicho kimeendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi.
Pamoja na washiriki wengine, hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa SAFAL Group, Anders Lindgren, Wakuu wa Wilaya wa Jiji la Dar es salaam, wadau na wafanyakazi kutoka ALAF.