Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali inaimarisha huduma za kiuchumi mkoani Mwanza kwa lengo la kuufanya Mkoa huo kuwa kituo kikuu cha biashara kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza na wananchi wa Mwanza leo Jumatatu Juni 14, 2021 akiwa njiani kwenda wilayani Misungwi, Rais Samia amesema hata ujenzi wa ofisi ya kisasa ya Benki Kuu (BoT) jijini Mwanza kwa gharama ya zaidi ya Sh 42 bilioni imejikita katika lengo hilo.
Katika kutekeleza mikakati hiyo, Serikali inaimarisha huduma za kifedha na kijamii ambapo tayari zaidi ya Sh39.7 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi eneo la Nyegezi na soko kuu.
“Ni nia ya Serikali kuona Mwanza inakuwa kituo kikuu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki,” amesema Rais Samia.
Rais Samia yupo mkoani humo kwa ziara ya siku tatu aliyoianza jana Juni 13 na leo Juni 14 pamoja na mambo mengine, atafanya ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Daraja la JPM (Kigongo -Busisi), atafanya ufunguzi wa Mradi wa Maji Misungwi na kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tano (Mwanza hadi Isaka).