Serikali nchini, imeweka mkakati wa kupunguza athari zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa kwa kupikia ikiwemo za Kimazingira, Kiafya, Kijamii na Kiuchumi kwa kuandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Aprili 12, 2023 jijini Dodoma Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Seleman Jafo amesema kwakua watumiaji Wakubwa wa nishati za kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni Taasisi za Umma na Binafsi, dira hii imeelekeza usitishwaji wa matumizi ya kuni kwa taasisi hizo. 

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Seleman Jafo.

Amesema, “kwa Mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 13 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191, natoa Katazo Kwa Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo tarehe 31 Januari, 2024, Aidha, Taasisi zinazoandaa Chakula na kulisha watu zaidi ya mia tatu (300) kwa siku kusitisha matumizi ya Kuni na mkaa ifikapo 31 Januari, 2025.”

Aidha, Waziri Jafo amesema Taasisi hizo ziwe zinatumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia na kusema kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda, hivyo matumizi ya nishati Mbadala yatatoa fursa kwa viwanda kutengeneza mkaa mbadala na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya matumizi fanisi ya nishati hiyo. 

Eduardo Camavinga aishika pabaya Real Madrid
Kocha Rivers United aichimba mkwara Young Africans