Serikali inaandaa kitini kitakachotoa mwongozo wa jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yatakavyonufaika na misamaha ya kodi iliyopo kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Septemba 30, 2021jiji Dodoma wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) uliozikutanisha NGO zote zinazofanya kazi hapa nchini.

“Kuhusu msamaha wa kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanya kazi kwa hisani, tayari tumekamilisha kuandaa kitini kinachotoa mwongozo wa namna mashirika yasiyo ya kiserikali yatanufaika na misamaha ya kodi. Tuko kwenye hatua za mwisho,” amesema Rais Samia

“Tunafahamu kwamba kuna changamoto katika mifumo yetu ya kodi na pia zipo baadhi ya taasisi ambazo zinastahili kupata mikopo. Tumeanza kufanyia kazi masuala yote haya” amesema Rais Samia

Kauli hiyo ya Rais Samia imekuja baada ya Mwenyekiti wa Nacongo, Dk Lilian Badi wakati akiwasilisha risala yao kwa Rais Samia kwa kueleza changamoto mbalimbali zinazoyakabili mashirika yasiyo ya serikali.

Ambapo ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupatikanaji wa misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya serikali na changamoto ya upatikanaji na uhuishaji wa vibali vya ukaazi kwa raia wasio Watanzania.

“Changamoto hizi zikifanyiwa kazi zitasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuweza kuchangia maendeleo kwa taifa kwa kushirikiana na serikali,” amesema Dk Badi

Aidha kuhusu changamoto ya upatikanaji wa vibali, Rais Samia amesema sasa kuna mfumo wa kielektroniki ambao umepunguza urasimu na vibali vinapatikana haraka ndani ya siku moja hadi tatu tofauti na ilivyokuwa zamani.

“Nimeambiwa kwa sasa endapo mwombaji atakuwa amekamilisha taratibu zote, anapata vibali katika kipindi cha siku moja hadi tatu kutoka siku 14 na zaidi zilizokuwa hapo nyuma. Hivyo kwa sasa kazi imebaki kwa waombaji kuwasilisha maombi yaliyokamilika,” amesema kiongozi huyo.

Hotuba ya Rais Samia yatajwa kwenye Hotuba Bora za UN
Young Africans yaifuata Geita Gold