Serikali imesema inatarajia kukopa Sh7.34 trilioni kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara.
Kati ya kiasi hicho, Sh4.99 trilioni ni mikopo ya ndani ambayo inajumuisha Sh3.15 trilioni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Sh1.84 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha bajeti ya serikali leo Alhamisi Juni 10, 2021 bungeni mjini Dodoma Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Sh2.35 trilioni zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kwa mwaka 2021/22 Serikali inapanga kutumia Sh36.33 trilioni kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo Sh23 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh13.33 trilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.”
“Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha Sh10.66 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, Sh8.15 trilioni kwa ajili ya mishahara na Sh4.19 trilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo,” amesema.
Amesema Serikali imetenga Sh200.0 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.