Wizara ya Maliasili na Utalii imetakiwa kuendelea kutumia sheria na taratibu zilizopo kulinda Wanyama waliohifadhiwa katika hifadhi za Taifa pamoja na mapori ya akiba nchini.
Wito huo, umetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Mwanga, Joseph Anania Thadayo katikakipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu ambapo alitaka kujua kuwa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inapitia upya sheria za uhifadhi ambazo ziliwekwa kwa ajili ya kulinda uhifadhi.
Katika swali la Mbunge huyo, pia alitaka kufahamu sheria hizo ni kwa namna gani zinawalinda wananchi ikiwemo kujitoa kwenye baadhi ya mikataba ya Kimataifa ambayo inashurutisha kuweka sheria ambazo zinawadhuru raia na mali zao.
Akijibu maswali hayo, Majaliwa alisema kumekuwa na taarifa mbalimbali zikieleza uwepo wa usumbufu kwa Wananchi kutoka kwa Wanyama wakali na waharibifu, hasa wale wanaoishi pembezoni na maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori.
Amesema, kwa kutumia sheria zilizopo Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kulinda wanyamapori pamoja na wananchi wanaozunguka kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutumia sheria zilizopo.