Wiki ya Unyonyeshaji watoto maziwa ya mama duniani imeanza rasmi chini ya kauli mbiu isemayo ‘Kuongeza Unyonyeshaji: Elimisha na Usaidizi’ huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito kwa Serikali kutenga rasilimali zaidi ili kulinda, kukuza, na kusaidia sera na programu za unyonyeshaji, haswa kwa familia zilizo hatarini.

Wito huu umetolewa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto UNICEF na la Afya ulimwenguni WHO, ambayo kwa pamoja wameeleza maziwa ya mama ndio chanjo ya kwanza inayomlinda mtoto kutopata magonjwa ya kawaida ya utotoni, kutopata utapiamlo na udumavu.

Katika taarifa yao ya pamoja kutoka New York Marekani na Geneva Uswisi mashirika hayo yametolea mfano wakina mama walio katika Pembe ya Afrika, Ukanda wa Sahel, Afghanistan, Yemen na Ukraine kuwa wengi wao wanashindwa kuwahakikishia watoto wao unyonyeshaji.

“Na hiyo hupelekea watoto wengi kukumbwa na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa kushindwa kunyonya maziwa ya mama kama chanzo salama cha lishe kwakuwa wazazi wao ni wachovu wa kimwili, wanakosa faragha, usafi ni duni na muda wote wapo kwenye hali ya dharura,” yamesema mashirika hayo.

Aidha, UNICEF na WHO wanatoa wito kwa Serikali, wafadhili, mashirika ya kiraia na sekta binafsi kuongeza juhudi kwenye kuweka kipaumbele kwenye programu za usaidizi wa unyonyeshaji, kuhakikisha wanawapa wahudumu wa afya lishe na ushauri bora.

Wamesema, “Tuwasaidie akina mama wanaonyonyesha, kutekeleza sera zinazofaa na zenye kuhakikisha wakina mama kupata nafasi na usaidizi unaohitajika kunyonyesha, na kulinda walezi na wahudumu wa afya wasi washawishi wanyonyeshaji kutumia maziwa ya kutengenezwa viwandani.

Katika hatua nyingine, mashirika hayo yametangaza takwimu zinazoonesha chini ya nusu, ya watoto wote wanaozaliwa, hunyonyeshwa katika saa ya kwanza ya maisha yao, na kuwaacha katika hatari zaidi ya magonjwa na kifo.

Baraza la afya ulimwenguni, nalo liliweka malengo ya kunyonyesha watoto bila kuwapa kitu kingine chochote kwa miezi sita wafikie asilimia 50 ifikapo mwaka 2025 lakini takwimu zilizotolewa leo zinaonesha ni asilimia 44 pekee ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza.

Wakati mizozo ya kimataifa ikiendelea kutishia afya na lishe ya mamilioni ya watoto ulimwenguni, umuhimu wa kunyonyesha kama mwanzo bora zaidi maishani umezidi mara dufu kuliko hapo awali.

Serikali yatoa tahadhari virusi vya Monkeypox
Katibu mkuu UN amuomba radhi Rais wa DRC