Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini (Export Permit) badala ya vibali hivyo kutolewa ofisi ya Waziri wa Kilimo kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 20,2021 kwenye ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam kukagua hali ya upakuaji wa mbolea, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema vibali hivyo pia vitatolewa kwa njia ya mtandao (Online) hivyo Wizara itakuwa na jukumu la kupokea taarifa kutoka TFRA.
Waziri Mkenda amesisitiza kuwa Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha inadhibiti ongezeko la bei ya mbolea, huku akiwahasa wafanyabiashara wa mbolea waliohifadhi ili kuiza kwa gharama kubwa kuacha mara moja kwani suala hilo halitaweza kutokea kwasababu mbolea kwasasa nchini inaingia kwa kiasi kikubwa.
Aidha bei ya mbolea kwenye soko la Dunia imepanda kwa kiasi kikubwa hivyo serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa bei ya mbolea nchini inaendelea kuwa katika ustahimilivu wa bei huku juhudi zikiendelea za kuhakikisha bei ya mbolea inashuka bei.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Wizara yake tayari imefanya mazungumzo na Uongozi wa Bandari ya Dar es salaam ili kuhakikisha kuwa mbolea inapowasili bandarini inapewa kipaumbele ili iweze kupakuliwa kwa haraka na kuwafikia wakulima kwa wakati.