Wizara Maliasili na Utalii inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufukua nyayo za Laetoli zilizopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro zilizogunduliwa na mtafiti Dkt. Mary Leakey mwaka 1978.
Jitihada hizo za wizara zinafanywa kutokana na agizo la Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete mwaka 2007, alipoitaka wizara hiyo kufukua nyayo hizo na kuzi hifadhi kwa njia za kisasa kwa matumizi ya elimu na utalii kwa Watanzania na wageni.
Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ramo Makani, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Hawa Mchafu Chakoma (CCM), aliyetaka kujua serikali inafanya mkakati gani kuajiri wataalamu wa kufukua nyayo hizo.
Makani amesema, mradi huo una gharama kubwa na unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 50 (sawa na Sh bilioni 105), ambazo zitatumika kwa ajili ya kusomesha wataalamu na kuandaa michoro ya ujenzi wa makumbusho.
Pia fedha hizo zitatumika katika kufufua na kuhifadhi nyayo hizo, kusimamia ujenzi na kuweka mifumo ya uhifadhi wa kisasa wa nyayo hizo.
Amesema fedha hizo ni nyingi, ukilinganisha na mapato na majukumu ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ambayo inatakiwa kugharamia, hivyo wizara inaendelea kutafuta fedha ili kugharamia utekelezaji wa mradi huo.
Hata hivyo, Makani amesema hakuna hali ya kusuasua katika kutekeleza mradi huo kwani baadhi ya kazi tayari zimesha kamilika na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, kazi zilizokamilika ni pamoja na kuundwa kwa idara ya urithi wa utamaduni, kukamilika kwa michoro ya awali ya jengo la mapokezi, jengo la utafiti na jengo la elimu kwa umma.