Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) ametishia kuwa endapo wananchi wake hawatopata maji kutoka chanzo cha maji cha Ihelele kama walivyo ahidiwa na serikali, ataongozana na wananchi hao kwenda kuzima mitambo ya maji katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, chanzo hicho cha maji kwa sasa kinazalisha maji yanayo pelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Shinyanga na Kahama kupitia Mamlaka ya Maji safi na Mazingira Kahama na Shinyanga (Kashuwasa).
Amesema hayo wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni Dodoma, mbunge huyo ameisema tangu serikali iahidi kuwa jimbo hilo la Misungwi litapata maji kupitia mradi huo wa maji wa Ihelele hadi sasa maji hayo hayatoki wakati maeneo mengine yanapata.
“Naibu Spika nasema wazi kuwa nitaongozana na wananchi wa jimbo langu kwenda kuuzima ule mtambo wa maji Ihelele kama maji haya yataendelea kutotoka kwenye maeneo yetu,” amesema Kitwanga ambapo alishangiliwa sana na wabunge wenzake.
Hata hivyo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amemtaka mbunge huyo asiandamane na wananchi wake, kwani kilichokwamisha maji hayo yasifike jimboni kwake ni uhaba wa fedha za kuunganisha bomba la maji hadi eneo hilo ambapo zinahitajika takribani Sh. bilioni nne.

Serikali kutumia bilioni 105 kutunza nyayo za binadamu wa kale
Yanga Kulipa Kisasi Leo?