Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameametoa wiki tano kwa kamati aliyoiunda kushughulikia upatikanaji wa eneo la wachimbaji wadogo katika leseni ya utafiti wa makaa ya mawe.
Agizo hilo amelitoa mara baada ya kuunda kamati hiyo baada ya kutembelea eneo linalomilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), na Kampuni ya Maganga Mtitu International (MMI), lililopo kijiji cha Katewaka Wilayani Ludewa Mkoani Njombe.
Amesema, kwa muda uliotolewa Kamati itafute namna bora ya kuwapatia eneo wachimbaji wadogo wa madini ya makaa ya mawe, shaba na dhahabu na kuwaelimisha kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kupatiwa leseni na mikopo ya kuendeshea shughuli za uchimbaji wa madini.
“Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi watendaji wake kuwalea wachimbaji wadogo na kuhakikisha kila mahali penye madini tunatenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo,” amesisitiza Naibu Waziri huyo wa Madini.
Kamati hiyo inahusisha mjumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Ludewa, Ofisi ya Mkurugenzi wa NDC, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ludewa na Kampuni ya Maganga Mtitu International.