Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imemfukuza nchini humo Balozi wa Umoja wa Ulaya, Bart Ouvry baada ya kuchukizwa na uamuzi wa Umoja huo dhidi ya viongozi wake.
Serikali imetangaza uamuzi huo ikitoa saa 48 kwa mwanadiplomasia huyo kuondoka nchini humo, wakati nchi hiyo ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu Jumapili wiki hii.
Uamuzi huo uliotangazwa jana umetokana na kile ambacho Serikali ya DRC imekielezea kama ukandamazaji baada ya Umoja wa Ulaya kuwaongezea vikwazo maafisa wake waandamizi ikiwa ni pamoja na mgombea urais kwa tiketi ya chama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary.
Shadary, ambaye ni Waziri wa zamani wa mambo ya ndani amewekewa vikwazo vya kutoingia katika nchi za Umoja wa Ulaya.
Msemaji wa Umoja wa Ulaya ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanasikitishwa na hatua hiyo ambayo wameitaja kuwa kinyume cha haki.
“Katika siku chache kabla ya uchaguzi ambao una ushindani na changamoto nyingi, uamuzi huo sio wa haki,” alisema.
Mwanadiplomasia Ouvry alikuwa balozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo tangu Desemba 2016.