Msemji wa serikali ya Uganda, Ofwno Opondo amesema kuwa Raisi wa Marekani Donald Trump anapaswa kutatua na kurekebisha matatizo ya taifa lake badala ya kuingilia maswala ya nchi ya Uganda.
Opondo alikuwa akijibu ujumbe wa raisi Trump ulioandikwa kwenye ukurasa wake wa Twitter uliosema kuwa watu hawataona Uganda ni sehemu salama hadi pale watekaji nyara wa raia wa Marekani Kim Sue Endicott pamoja na mwenzake,Jean-Paul Mirenge raia wa Congo watakapokamatwa.
Watekaji hao waliwakamata watalii hao kwa mtutu wa bunduki huku wakidai kulipwa Dolla za kimarekani 500,000 sawa na zaidi ya shilingi bilioni moja ya kitanzania.
Kupitia ukurasa wake wa twitter, Opondo amejibu akisema kuwa kuna vifo vingi vinavyotokana na matumizi ya bunduki nchini Marekani kulinganisha na matukio ya nadra ya utekaji nyara yanayotokea Uganda, aliongeza kuwa Uganda itaendelea kuimarisha hali yake ya usalama.
Hata hivyo kufuatia utekaji nyara huo Rais Trump alisema kuwa kitendo hicho huenda kikaathiri sekta ya utalii Uganda ambapo amewataka watekaji hao wakamatwe kabla ya wamarekani kuzuru taifa hilo.
Awali Rais wa Uganda Yoweri Museven alitweet akisema kuwa taifa lake lipo salama kwa Raia wa Uganda na watalii huku akiwalaumu wahalifu wachache kwa kuichafua Uganda.
Wanajeshi na mamlaka ya wanyamapori Uganda na kitengo cha polisi wa utalii kwa pamoja walifanya opareshini ya pamoja ili kuwaokoa mateka Endicott na Mirenge.
Baadhi ya vyombo vya habari vya nje vimeripoti kuwa wawili hao waliachiwa siku ya jumapili mara tuu baada ya fedha zilizotajwa kuwakomboa kulipwa kwa watekaji.
Hata hivyo msemaji wa serikali ya Uganda alituma ujumbe twitter na kusema kuwa waliokolewa na vikosi vya Serikali ya Uganda nchini Jamhuri ya Kidemokerasia ya Kongo (DRC) na walikuwa salama salmini mpakani mwa DRC na Uganda.