Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza mafuta nchini kwa kufungua kituo cha kwanza kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha Serikali kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta ( TANCOIL).
Kalemani amesema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika lake la TPDC,kuwapatia na kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.
Uzinduzi huo pamoja na kufungua kituo hicho vimefanyika wilayani Musoma, mkoani Mara Juni 6, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa huo, akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara hiyo na Taasisi zilizochini yake.
Amesema baada ya kuanza rasmi kwa biashara hiyo, TPDC kupitia TANCOIL itashirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya Serikali ya kufungua na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.
Amebainisha kuwa serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo hivyo: Aidha itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini yanasimamiwa TPDC.
“Watanzania tutembee kufua mbele na kujivunia vilivyo vya kwetu! Uzinduzi wa biashara hii ya mafuta hapa Musoma leo unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ya Uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli, ni kutambua juhudi na mchango mkubwa wa Baba wa Taifa,. Alisisitiza Dkt. Kalemani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini, (TPDC), Dkt. James Mataragio alisema kuwa katika kutekeleza azma hiyo ya serikali, kuanzia mwaka huu wa fedha 2020/2021, TPDC imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya mtaji wa kugharamia shughuli za uagizaji, usambazaji na usimamizi wa mauzo ya mafuta nchini kote.