Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema inaangalia uwezekano wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Benjamini William Mkapa iliyopo jijini Dodoma ili iwe hospitali ya Taifa badala ya kuendelea kubakia kuwa ya kanda.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akimkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzungumza na waashiriki katika uzinduzi wa huduma za kibingwa za upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant) hasa kwa watu wenye Seli Mundu (Sickle Cell).
Amesema, “Tumeanza kujenga kituo cha kutoa tiba ya kansa na pia tunataka tujenge kituo cha umahiri cha matibabu ya moyo ili kuimarisha utoaji wa huduma kwenye hospitali yetu.”
Alisema kufanyika kwa upandikizaji wa uloto kwenye hospitali hiyo, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa nchi saba zinazotoa huduma hiyo barani Afrika na Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanza kutoa huduma hiyo.