Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya kufanya kampeni ya kutosha katika kuhamasisha matumizi ya vyandarua vya kisasa hadi maendeo ya vijijini nakuhakikisha afua hiyo inaanza kutekelezwa katika Mikoa yenye kiwango cha maambukizi chini ya asilimia moja, ili kuharakisha ufikiwaji wa malengo ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria hapa nchini.
Majaliwa ameyasema hayo wakati alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2023 yaliyofanyika Kitaifa Jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Naipongeza Wizara ya Afya kwa dhamira ya dhati katika mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania. Hivi sasa, zaidi ya 98% ya kesi za malaria zinathibitiwa, kesi za malaria zilizothibitiwa kwa mwaka zinaonesha kati ya kila watu 1,000 zilipungua kutoka 106 mwaka 2020 hadi 76 mwaka 2021 na zaidi hadi 58 mwaka 2022.”
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa, mikoa inayoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria ni Tabora una asilimia 23, Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara una asilimia 15.