Serikali imehimiza kukamilishwa kwa wakati, ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Nyakanazi ili pamoja na manufaa mengine, kiwaondolee wananchi wa mkoa wa Kagera, adha ya kutokupata umeme wa kutosha.
Kamishna msaidizi wa umeme kutoka wizara ya nishati, mhandisi Innocent Luoga amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa na serikali kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya L & T Construction kutoka India ni kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Februari 2021, kama ilivyo kwenye mkataba.
“Mathalani, ili mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Rusumo hadi hapa Nyakanazi, umbali wa kilomita 94, uweze kufanya kazi, unategemea mradi huu wa kituo cha kupoza umeme ukamilike,” amesema Luoga.
“Pia, unahusisha mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Geita mpaka hapa Nyakanazi, umbali wa kilomita 54,” ameongeza Luoga .
Akifafanua zaidi kuhusu manufaa ya kituo hicho, Luoga amesema kukamilika kwake kutasaidia kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera ambayo itaingizwa katika gridi ya taifa.
Aidha, amesema kuwa tafsiri ya uwepo wa umeme wa uhakika inamaanisha shughuli za kijamii na kiuchumi zitaboreshwa hivyo pato la taifa litaongezeka.