Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amesema Serikali inajivunia kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR kufikia malengo ya 95/95/95 ifikapo mwaka 2025.
Majaliwa ameyasema hayo wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yaliyowezeshwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) iliyofanyika katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Hivi sasa kupitia mpango wa PEPFAR tunatekeleza tafiti ya athari za VVU Tanzania kwa mwaka 2022-2023 ambao unakusudiwa kutoa taarifa muhimu katika kuandaa mikakati ya kuzuia maambukizi mapya na kuhakikisha watu wanajua hali zao za VVU.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa PEPFAR Tanzania, Jessica Greene alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma unaongezwa kwa wasichana, wanawake vijana, watoto na makundi ya jamii yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa VVU.
Tangu kuanzishwa kwa PEPFAR mwaka 2003, chini ya utawala wa Rais George W. Bush, Serikali ya Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 100 katika kupambana na VVU/UKIMWI duniani kote, ikijumuisha takriban Dola za Kimarekani bilioni saba zilizotolewa Tanzania.