Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa majibu kuhusu taarifa za mgogoro wa utekelezaji wa ununuzi wa ndege ya tatu inayonunuliwa na Serikali ya Tanzania kutoka kampuni ya Bombadier ya Nchini Canada.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo na Serikali kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu imeeleza kuwa ni kweli mgogoro huo upo ila kimsingi ni mgogoro ambao umetengenezwa na Watanzania ambao kwa bahati mbaya sana wameweka maslahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya maslahi ya Taifa.
Hivyo, Serikali imesema kuwa ndege hizo zinazonunuliwa ikiwepo hiyo ambayo imetengenezewa mizengwe na sio ya Rais Magufuli bali ni za watanzania wote.
Baadhi ya viongozi wa kiasiasa wanaoshabikia migogoro inayokumba jitihada za Rais Magufuli, za kutuletea maendeleo, hawana uzalendo.
Serikali imeeleza kusikitishwa sana tena sana kwa hujuma zinazofanywa waziwazi tena kwa ushabiki wa hali ya juu na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa chama hicho, kupingana na mwelekeo mzuri wa Rais kutuletea maendeleo.
“Kwa mtu yeyote mwenye uchungu na nchi yake, angepambana ili jambo linalohusu maslahi ya Taifa, likiwepo la kununua ndege, lisikwame na kama kuna mkwamo basi ashiriki kukwamua badala ya kushabikia.
Serikali pia ina fununu kwamba watu hawahawa wanaohujumu jitihada za kimaendeleo, pia wanahujumu hata hali ya usalama wa raia wetu kwenye baadhi ya maeneo ya Nchi yetu. Hili nalo linaendelea kufanyiwa kazi kwa kina.
Wanaopinga mambo ya Maendeleo hawapingani na Mhe. Magufuli bali wanapingana na Watanzania wote kwa ujumla.
Hivyo basi ni vyema Watanzania mkaelewa ukweli wa hali halisi na mkapuuzia mambo ambayo yanashabikiwa na baadhi ya viongozi hao wa kisiasa wanaotafuta umaarufu rahisi (Cheap Popularity). Endeleeni kumuombea Rais wetu na Tanzania kwa Ujumla kwani Chini ya Uongozi wake, amedhamiria kwamba hakuna kurudi nyuma (no reverse gear).
Serikali ilikuwa inawahisi baadhi ya wanasiasa kuhusika na hujuma hizi na sasa sio hisia tena bali baadhi yao wameshaanza kujitokeza hadharani.”
Serikali imezitaja hatua mbalimbali inazochukua kuhusiana na mgogoro kwenye ununuzi wa ndege, zikiwepo hatua za kidiplomasia na za kisheria ili kumaliza jambo hili.
Aidha, kwa wale wanaoshabikia na kutengneza migogoro na hujuma mbalimbali dhidi ya maendeleo ya Tanzania, Serikali itaendelea na taratibu za kiuchunguzi na haitasita kuchukua hatua za kisheria zinazostahili.
“Serikali inatumia pia fursa hii kuwaomba Watanzania wasiwe na wasiwasi wala tashwishi kuhusu mpango wa Ndege kununuliwa na kwamba waendelee kuiamini Serikali yao iliyopo madarakani inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Uzalendo wetu uwe ndio mtaji mkubwa kuliko siasa, dini au ukabila.”
Serikali imesema kuwa imepata fununu kwamba kuna viongozi wa baadhi ya Vyama vya Siasa ambao kwa namna moja au nyingine wangependa kuhujumu jitihada za Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kuwaletea Watanzania (hasa wanyonge) maendeleo.
Msemaji huyo ameeleza kuwa wanasheria hao waliokwenda kufungua madai kwamba Serikali yetu inadaiwa na kwamba ndege hiyo ishikiliwe, hawana uhalali wowote wa kufanya hivyo na ni matapeli tu ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wasioitakia mema Tanzania.
Amesema kuwa sasa watu hao wamejidhihirisha hadharani kwamba wao ndio wako nyuma ya pazia la kuhujumu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa maslahi yao ya kisiasa.
Hivyo Serikali ya awamu ya Tano inawahakikishiwa Watanzania kwamba ndege itakuja. “Wanaokwamisha jitihada za Serikali za kuleta ndege watapanda na ndugu zao watapanda na wafuasi wao watapanda.”
Pia amesema kuwa, Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli haibagui watanzania kwa itikadi za Kisiasa, Dini, Kabila, rangi au utofauti wowote.