Serikali nchini, imelaani vikali kufuatia matukio ya Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu kuvamiwa na kuuawa na wananchi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao kisheria.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana jijini Dodoma wakati alipokuwa akijibu hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Amesema, kuanzia Machi mwaka jana hadi Februari mwaka huu jumla ya askari wa Uhifadhi na Watumishi 9 wameuawa huku jumla ya Askari wa Uhifadhi na Watumishi 68 wakijeruhiwa.
“Baadhi ya wananchi wanapokamatwa kwa makosa ya kuingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria wana tabia ya wananchi kujipanga na kuvamia askari au kambi zao na kuwashambulia kwa silaha mbalimbali za jadi kama vile fimbo, sime, mapanga na mishale,” amesema Balozi Chana.
“Matukio haya yamekuwa yakijrudia mara kwa mara katika maeneo mbalimbali hapa nchini na mara nyingi yamekuwa yakitokea pindi askari wa Jeshi la Uhifadhi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi” ameongeza Waziri huyo.
Aidha ameongeza kuwa, “matukio haya yamepelekea askari wa Jeshi la Uhifadhi kujeruhiwa au kuuwawa pamoja na kusababisha uharibibifu wa mali za Serikali kama vile kuchoma moto magari, nyumba na vitendea kazi vingine muhimu kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.”