Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, linamshikilia Godfather Mndeme (36), mkazi wa Kijiji cha Mikungani katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, kwa tuhuma za kumuua mkewe, Furaha Akashi (40) kisha kumfukia kisimani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justin Maseju amethibitisha kutokea na kubainisha kuwa wanawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuhusika na tuhuma hizo za mauaji yaliyopangwa kabla na baada ya utekelezaji wake huku akisema, “Kweli tukio limetokea na tunawashikilia watu wawili akiwamo mume wa marehemu wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo,” amesema Kamanda Maseju.

Wiki tatu zilizopita, Mndeme anadaiwa kumuua mkewe na kumfukia katika kisima hicho kisha kupanda mti na kumuajiri mtu awe anaumwagilia maji na kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mikungani, Idd Salum alisema mauaji hayo yanadaiwa kutekelezwa Januari 7 na walipolibaini hilo walilazimika kuufukua mwili wa marehemu ambao ulizikwa tena Januari 29 baada ya kukamilishwa na utaratibu wa kiuchunguzi na hatua za kisheria.

“Majirani hao walisema walimuuliza Mndeme kwa nini anatoa vyombo ndani na wakataka kujua alipo mkewe na akawajibu kuwa amesafiri kwenda Arusha hivyo anamfuata ila wakamzuia,” alisema mwenyekiti huyo na alisema majirani hao walienda kutoa taarifa ofisi ya kijiji hivyo akalazimika kufuatilia huku akimhoji Mndeme asema ukweli ili waweze kumsaidia kwani mke wake hakuonekana kwa muda mrefu kijiji hapo halafu ghafla anaonekana akihamisha vitu.

“Baadhi ya watu walitaka kumpiga huyo bwana ila alikiri kuwa amemuua mke wake baada ya kugombana na akaenda kutuonyesha alipomfukia ndipo tukatoa taarifa kituo cha polisi kwa hatua zaidi, Madaktari walibaini mwanamke huyo alipigwa na kuwekewa mti mgongoni kisha akafungwa na kumpiga kifuani, kichwani na kuvunjwa mguu,” alisema Salum.

Walipomaliza kufanya uchunguzi huo, alisema askari walitoa kibali cha mwili huo kuzikwa nao walimzika mahali alipokuwa amefukiwa na mumewe baada ya kumwita mchungaji aliyefanya sala na kumzika upya usiku.

Viongozi wa Kikanda wajadiliana kuwakabili Al-Shabab
Rais Samia ataja mikakati urekebishaji mifumo ya haki