Serikali imesema kuwa mpaka sasa imelipa zaidi ya shilingi bilioni 83 kwa wakulima wa Korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, pamoja na Ruvuma huku zaidi ya wakulima 82,835 kutoka mikoa hiyo wakiwa wamepatiwa fedha zao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ambapo amesema kuwa Jumla ya fedha iliyolipwa kwa wakulima hao ambao tayari wamefanyiwa uhakiki katika Mkoa wa Mtwara pekee ni 50,835, Lindi wakulima 22,131 na Mkoa wa Ruvuma ambao takribani wakulima 9,445 wamelipwa.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wabanguaji wadogo wa korosho wa mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Morogoro, ambapo amesema jumla ya vyama 328 vimefanyiwa uhakiki kati ya vyama 504 vilivyopo katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, jumla ya vyama 319 vimekwishalipwa.

Aidha, amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kujadiliana na kukubaliana utaratibu uliopangwa na serikali katika ubanguaji wa korosho mwaka 2018/2019 kwa kuelekeza ubanguaji kufanyika nchini ili kuwanufaisha wananchi katika ajira hiyo.

“Tumeiona changamoto ya mitaji kwa wabanguaji wadogo nchini sambamba na wabanguaji wakubwa hivyo ili serikali iwarahisishie upatikanaji wa mitaji tumeamua kuwapa kazi nyinyi wenyewe,” amesema Japhet Hasunga.

Hata hivyo, ameongeza kuwa suala la uhakiki limejikita zaidi kubaini udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wahujumu wa biashara ya korosho.

 

Ukusanyaji mapato wamchefua JPM
Serikali yafyeka mazao ya Wakulima