Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi tilioni 47.424 katika mwaka 2024/2025.
Dkt. Nchemba amesema hayo hii leo Oktoba 6, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 na kudai kuwa makusanyo hayo yatatokana na vyanzo mbalimbali yakiwemo mapato ya ndani, michango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na mikopo.
Amesema, “mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa shilingi tilioni 34.436 sawa na asilimia 72.6 ya bajeti yote, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi tilioni 4.291 sawa na asilimia 9.0 ya bajeti. Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 6.141 kutoka soko la ndani na shilingi trilioni 2.555 kutoka soko la nje.”
Aidha, Dkt. Nchemba alisema Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 imezingatia mwenendo wa ukusanyaji mapato, matarajio ya ukuaji wa uchumi, hali ya uchumi wa dunia pamoja na mikakati ambayo Serikali inaendelea kuchukua katika kuongeza mapato ya ndani.
Kuhusu matumizi ya Serikali kwa mwaka 2024/2025, Dkt. Nchemba alisema Serikali inakadiria kutumia shilingi tilioni 47.424 kati ya kiasi hicho, deni la Serikali shilingi tilioni 12.101, mishahara shilingi tilioni 11.774 na uendeshaji wa shughuli za Serikali shilingi tilioni 8.223.