Katika kuhakikisha kuwa Pombe aina ya viroba zinatkomezwa nchini, Serikali imefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na Uingizaji wa aina 20 ya pombe kali za viroba zilizokuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa Serikali imeamua kufuta leseni za uzalishaji na uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe zilizofungwa katika mifuko ya plastiki (Viroba).
“Tumefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na uingizaji kutoka nje, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa katika mifuko ya plastiki (viroba) chini ya ujazo wa milimita 200,” amesema Ummy Mwalimu.
Aidha, amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa tamko la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa Februari 02, 2017 la kusitisha uzalishaji, uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hiyo kali kuanzia Machi 01, 2017.
Ummy amesema kuwa usitishaji huo unazingatia kanuni za kukataza uzalishaji, uingizaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki kufungashia pombe kali za mwaka 2017 (The Environmental Management) imekatazwa kutumia vifungashio vya plastiki kufungashia pombe kali. Badala yake wazalishaji watapaswa kufungasha pombe kali hizo katika chupa zenye ujazo usiopungua mililita 200.
Hata hivyo, Ummy amesema kuwa Viroba vilivyokamatwa na kuzuiwa vinasubiri maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu namna ya kuviteketeza