Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Salum Mayanga amewateua viungo Himid Mao Mkami wa Azam FC na Jonas Gerald Mkude wa Simba, kuwa Manahodha wasaidizi wa timu hiyo.

Uteuzi unafuatia aliyekuwa Nahodha Msaidizi na Nahodha wa kikosi cha wachezaji wa nyumbani, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kuwa majeruhi tangu Januari mwaka huu.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema kwamba Mayanga ataendelea kumtumia mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Ally Samatta kama nahodha mkuu.

“Mabadiliko hayo yamefanyika kwa wasaidizi pekee, hivyo Samatta ataendelea na majukumu yake katika mechi za AFCON, Kombe la Dunia na za kirafiki za kimataifa, wakati Mkude na Mao watakuwa Manahodjha wa kikosi cha CHAN,” alisema Lucas.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi mbili, kwanza na Botswana Machi 25 na baadaye Burundi Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na pamoja na Samatta, mchezaji mwingine wa Tanzania anayecheza Ulaya, Farid Mussa anatarajiwa pia kuwasili leo.

Kikosi kamili cha Stars kwa ajili ya mechi hizo, ambacho kimeingia kambini hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Azam FC), Deogratius Munishi (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia aliwataja Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael (Azam FC).

Walinzi wa kati Vicent Andrew (Yanga SC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Erasto Nyoni (Azam FC) ilihali aliwataja viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude (Simba SC).

Kadhalika wako viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Frank Domoyo (Azam FC) na Muzamil Yassin (Simba) wakati viungo wa kulia waliotajwa ni Simon Msuva (Yanga SC) na Shizza Kichuya (Simba SC).

Viungo wa kushoto ni Farid Mussa (Teneriffe, Hispania) na Hassan Kabunda (Mwadui FC) wakati washambuliaji ni Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ibrahim Hajib (Simba SC), Mbaraka Yussuf (Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting).

Mayanga anasaidiwa kocha wa Makipa, Patrick Mwangata; Meneja wa timu, Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu wakati Daktari wa timu atakuwa Richard Yomba huku Daktari wa viungo akiwa ni Gilbert Kigadya.

Sumaye atoa ya moyoni kuhusu Serikali ya awamu ya Tano
Serikali yapigilia msumali uzalishaji wa pombe aina ya viroba