Waziri wa mambo ya ndani wa Uganda, Meja Jenerali Kahinda Otafiire amesema amedhamiria kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha raia wanaokwenda kufanya kazi za nje barani Asia wanalindwa dhidi ya kudhurika na kuchukuliwa viungo vyao vya kimwili kinyume cha sheria.
Meja Otafiire, ameyasema hayo wakati akijibu swali la mwandishi kuwa ni kwanini kati ya hospitali zote nchini humo alichagua Hospitali ya Victoria kufanya uchunguzi wa kina wa viungo vya ndani kwa wale wote wanaokwenda kufanya uchungu wa nje.
Amesema, amekuwa akipata taarifa za Waganda ambao wanapelekwa katika Hospitali hiyo kisha kufichwa kwa madai ya kupewa ajira lakini huishia kunyofolewa viungo vyao kwa uhalifu na maiti zao kurushwa mto ili ziliwe na mamba.
Kwa mujibu wa Meja Otafiire, amesema asafirishaji wengi wa vibarua wamekuwa wakitumia kliniki kupata matokeo ghushi ambayo wanayatumia kuwapeleka watu kufanya kazi nje ya nchi.
Amesema, “Mara tu vibarua hao wanapofika katika nchi kama Saudi Arabia, baadhi hupelekwa sehemu nyingine, na hapa Thailand ilitajwa, ambapo viungo vyao vinatolewa na kisha miili yao kuwa chakula cha mamba.”
“Kazi yako ya kusafirisha nje ni kutafuta pesa huku unapata pesa, na mimi kazi yangu ni kuwalinda Waganda, huwezi kuuza Waganda wakati tunaona na juu ya hili, hakuna maelewano tutawashika wote,” amesema Waziri huyo.
Ameongeza kuwa, “Wanakupeleka tu hadi Saudi Arabia, kukupeleka mahali pengine kama Thailand, wanachukua moyo wako, figo au ini na kutupa mwili wako kwa mamba na wewe unataka nisikie hivyo nikae kimya? sitaenda mbinguni.”
Hata hivyo, Otafiire hakutoa idadi ya Waganda wanaoaminika kupoteza viungo vyao vya mwili kwa wasafirishaji au wameuawa na kulishwa kwa mamba ambapo pia hakutaja maeneo ambayo uvunaji wa viungo vya mwili unafanyika ili kuepukwa.