Waziri wa maji, Profesa Makame Mbarawa amesema kuanzia sasa amesitisha kutoa vibali vya ujenzi wa miradi ya maji kwa wakandarasi kutokana na wengi wao kuwa wadanganyifu katika makadirio ya gharama za utekelezaji wa miradi hiyo na kusababishia Serikali mzigo mzito, mkubwa na kukwama kwa miradi mingi.
Ametoa agizo hilo akiwa ziarani mkoani Lindi akitembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maji katika Manispaa ya mji wa Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maji inaendelea kwa kasi na kukamilika kwa wakati.
Mbalawa amesema kuwa amegundua kuna tabia ya wakandarasi wengi wasio waadilifu kuweka gharama kubwa ili kupata faida kubwa, hivyo ameamua kusitisha vibali vya ujenzi kwa wakandarasi na kutoa kazi hizo kwa Wakala wa Usamabazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), pamoja na mamlaka za maji.
Amefafanua kuwa maamuzi hayo yamelenga kukomesha tabia hiyo ya wizi wa fedha za Serikali na kuokoa fedha nyingi zinazoweza kutumika katika utekelezaji wa miradi katika maeneo mengine.
Katika hatua nyingine, Mbalawa amemtaka Mkurugenzi wa Manispaaa ya Lindi na mkandarasi wa kampuni ya M/S Halem Construction co. Ltd wakae chini na kufikia makubaliano na kuiacha Wizara ya Maji ifanye utaratibu wa manunuzi ya bomba za kusambaza maji kijijini Nandambi kwani mkandarasi huyo amonesha kusuasua.
Kwaupande wa wakazi wa kijiji cha Nandambi wamemueleza Waziri wa Maji kua hatua hiyo itakuwa na msaada mkubwa kwao ikizingitiwa kuwa mradi huo ulianza utekelezaji wake Agosti, 2018 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2019, lakini hauoneshi matumaini ya kukamilika.