Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema watu 2,160 nchini wamepoteza maisha kwa ajali ya pikipiki maarufu kama bodaboda kati ya mwaka 2016 na 2019.
Masauni ametaja idadi hiyo leo, Septemba 9, 2019 Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka aliyetaka kufahamu kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na zoezi la ukamataji wa pikipiki kutokana na kukiuka sheria na taratibu.
Naibu Waziri huyo amelieleza Bunge kuwa tangu Januari 2016 hadi Juni 2019, ajali 5,213 ziliripotiwa.
Aidha, alisema kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na ajali ya bodaboda iliongezeka mwaka huu kwa asilimia 6.6 kwa kulinganisha na mwaka uliopita.
Alieleza kuwa kati ya Januari na Juni mwaka huu, watu 176 walipoteza maisha kwa ajali ya pikipiki na 289 walijeruhiwa. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Masauni, katika kipindi kama hicho mwaka jana watu 165 walipoteza maisha na 344 walijeruhiwa.
Akitaja idadi ya ajali katika miaka yote mitatu, alisema mwaka 2016, ajali za pikipiki zilikuwa 2,544 na zilisababisha vifo vya watu 890 na majeruhi 2,128; mwaka 2017 ajali 1,459 na zilisababisha vifo 728 na majeruhi 694.
Dar24 kupitia kipindi cha On The Bench, mwaka huu iliwakutanisha bodaboda wa Wilaya ya Ilala na Mkuu wa Trafiki wa eneo hilo (DTO na Muwakilishi kutoka Taasisi ya Mabalozi wa Huduma za Usafiri Barabarani (RSA) ambapo kwa pamoja walizungumzia changamoto zilizopo ili kuboresha na kuepuka ajali.
Kipindi cha On The Bench hurushwa kupitia YouTube channel ya ‘Dar24 Media’ kila Jumanne na huwakutanisha viongozi, watalaam na wananchi wa kawaida ambapo hujadili changamoto zinazowakabili.