Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ametoa kibali kwa watumishi wa Mungu wa dini zote kuhubiri na kutangaza neno la Mungu sehemu mbalimbali kama vile klabu, Disko na Kumbi za starehe ili neno la Mungu lizidi kuenea na kuwafikia watu mahali popote walipo.

Ambapo amesema mtumishi yeyote atakapohitaji kuhubiri, muziki utazimwa kwa muda wa nusu saa na baada ya hapo watu wataendelea na starehe zao wakiwa tayari wamepokea neno la Mungu.

”Watumishi wa Mungu kama mnataka kuhubiri kwenye klabu, nawapa kibali mkawahubirie huko angalau kwa nusu saa wapate fursa ya kusikia neno la Mungu, wasije kusema hawakusikia, wafuateni huko,” amesema Makonda.

Ameongezea kuwa mmiliki wa klabu atakaemkatalia mtumishi Kuhubiri, RC Makonda atamuombea mtumishi huyo na ikibidi kumsindikiza.

”Mtumishi wa Mungu yeyote akitaka kwenda klabu ruksa, sasa nimuone huyo mwenye klabu akatae, mimi si ndiyo mkuu wa mkoa, kuanzia wiki ijayo mkitaka kwenda klabu yeyote mniambie” amesissitiza Makonda.

Makonda amesema hayo baada ya kubaini uwepo wa idadi kubwa ya watu kwenye sehemu za starehe na pindi watu hao wakienda makanisani na misikitini kuishia kusinzia na wengine wanakuwa wamechoka kiasi cha kushindwa kulisikiliza kwa ufasaha neno la Mungu.

Hayo yote yamejiri jana wakati alipokuwa akizungumza na maelfu ya waumini wa Kanisa la Arise and Shine linaloongozwa na mtumishi wa Mungu Apostle Boniface Mwamposa.

Video: Mbivu, mbichi Lissu, Ndugai leo | Nyumba 30 hatarini kuzama Dar
Mtoto wa miezi 5 akatwa kiganja, madaktari wadai damu ilivilia kumbe sumu