Serikali inakusudia kuanzisha utaratibu wa kulipa tozo katika mfumo mpya utakaoanza Julai Mosi, 2022, katika daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 17, 2022 wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile.
“Serikali imeendelea kupunguza tozo kwa watumiaji wa daraja la Kigamboni tangu kuzinduliwa kwake kwa kuzingatia tathmini ya uwezo wa wananchi kumudu tozo,” amesema Naibu Waziri.
Mbunge Ndugulile katika swali lake alitaka kujua ni lini mfumo mpya wa kulipia gharama hizo kwa siku, wiki hadi mwezi kwenye daraja la Kigamboni kwa wakazi wa jimbo lake.
Awali, katika swali la msingi, Dkt. Ndugulile aliuliza ni kiasi gani cha fedha kimekusanywa tangu daraja hilo kuanza kutumika na Serikali ina mpango gani wa kufanya huduma ya daraja hilo kuwa bure.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kasekenya, amesema mfuko wahifadhi ya jamii NSSSF, ulianza kupokea fedha zitokanazo na tozo kwa watumiaji wa daraja hilo Mei 14, 2016 baada ya kuzinduliwa rasmi.
“Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei,2022 mfuko huo ulikuwa umekusanya ShilingiBilioni 66.86 na kwamba mara ya mwisho Serikali kupunguza tozo za Daraja hilo la Kigamboni ilikuwa Mei 21, 2022,” amefafanua Kasekenya.