Serikali imesema kuwa upatikanaji wa dawa nchini umeongezeka katika hospitali, zahanati na vituo vya afya ambapo zinapatikana kwa asilimia 90.
Akizungumza kwa njia ya simu kupitia kituo cha redio cha Nyemo FM ya Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amesema kuwa ongezeko hilo la dawa linaenda sambamba na kupungua kwa bei ya dawa hizo ili kuhakikisha wananchi wanaweza kupata huduma bora za afya kwa bei wanayoimudu.
Bwanakunu amesema kuwa Serikali inaendelea kuwashawishi wawekezaji nchini kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza madawa kwani kuna soko kubwa nchini lakini dawa zinazotoka nje ya nchi zinaongeza gharama.
Bwanakunu ameongeza kuwa kwa sasa MSD inasambaza dawa kwa vituo mbalimbali vya upokeaji dawa vipatavyo 7514 na kutoa wito kwa vituo vya afya na hospitali kuagiza dawa mapema ili MSD iweze kuzisambaza kwa wakati. Ameongeza kuwa ili kuepuka gharama kubwa ya dawa zinazoagizwa kutoka nje, hivi sasa MSD inatekeleza agizo la Serikali kwa kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji badala ya kuwatumia wafanyabiashara ambao ni watu wa kati.
Akiongea katika mahojiano hayo maalum, Dkt. Abbasi ameeendelea kusisitiza kuwa mageuzi yaliyotokea katika kipindi cha miaka mitatu ni safari muhimu ya kuelekea Tanzania yenye neema.