Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye amesema kuwa msimamo wa Serikali katika kulinda kazi za filamu zinazouzwa nchini kuzingatia sheria na. 4 ya mwaka 1976 ya utengenezaji wa filamu na Michezo ya kuigiza.
Nnauye ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokutana na wadau wa filamu ikiwa ni mwendelezo wa Kipindi cha “Wadau Tuzungumze” kilichoandaliwa na Wizara kwa kuwashirikisha wadau wake wa kisekta.
“Ni wajibu kwa wanatasnia wa filamu kufuata sheria katika kuuza bidhaa zao bila kujali zimetoka nje ya nchi au ni za hapa hapa nchini ili kuwa na soko huru na la haki kwa filamu na michezo ya kuigiza” amesema Nape.
Aidha, Nape ameongeza kuwa ni wajibu wa kila mwanatasnia wa filamu kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano katika kutoa maoni ya kuandaa Sera ya filamu ambayo itakuwa mwongozo katika kuendesha na kusimamia kazi za filamu nchini.
Vile vile, Nape ameutaka uongozi wa Wizara kwa kushirikiana na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu kuhakikisha kuwa wanakutana na wadau ili kukamilisha uundwaji wa sera hiyo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini. Joyce Fissoo ameahidi kutekeleza agizo na kupanga kukutana na wadau wa filamu upande wa watayarishaji Februari 28 mwaka huu, ili kupata maoni kuhusu uundwaji wa sera ya filamu.
Hata hivyo, Msanii wa Filamu za kuigiza nchini, Single Mtambalike amewataka wadau wa filamu kushirikiana na serikali kwa kutoa maoni yao yatakayosaidia katika kukamilisha Sera ya filamu itakayotoa mwongozo thabiti kwa tasnia hiyo.