Mkurugenzi wa Habari Wizara ya Mambo ya Nje, Emmanuel Buhohela, amesema kuwa hawana taarifa rasmi kwamba Uingereza imepiga marufuku wasafiri kutoka nchini Tanzania kuingia nchini humo na kueleza kuwa hayo ni mambo ya mitandaoni.
Amesema hayo wakati akizungumza na kituo cha habari cha EATV, amabpo amesema kuwa serikali inautaratibu maalum wa kupokea taarifa hizo za namna hiyo na kwamba ingekuwa vyema zaidi kama Ubalozi wa Uingereza ungeulizwa kama hiyo kauli ni ya kwao.
“Utaratibu wa serikali ni kwamba kuna utaratibu wa kuwasiliana, kwahiyo hayo mambo ya kwenye mitandao hatuwezi kuyazungumzia, mimi binafsi nimeiona kama wewe ulivyoiona, serikali haiwasiliani kwenye mitandao bali ina utaratibu wake”, amesema Buhohela
“Kwenye mitandao mambo mangapi ya uongo yanayoandikwa, kama tukipata maandishi au document kutoka Uingereza tutalizungumzia, au mngewapigia Ubalozi wa Uingereza kuwauliza kama hiyo kauli ni ya kwao,” amesema Buhohela
Hii karibuni Katibu Mkuu wa Uchukuzi wa Uingereza Grant Shapps, kupitia ukurasa wake wa Twitter, aliandika kwamba zuio la wasafiri kutoka Tanzania na DR Congo, limeanza jana Ijumaa Januari 22, 2021, ikiwa ni hatua za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19, kufuatia kuibuka kwa kirusi kipya cha ugonjwa huo nchini Afrika Kusini