Serikali, imetoa taarifa rasmi kuhusu ugonjwa mpya unaotajwa kuenea Mkoani Lindi ambapo kwa hatua za uchunguzi wa awali imesema, sio Ebola, wala UVIKO 19.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema Julai 7, 2022, Wizara ya Afya ilipokea taarifa toka kwa Mganga Mkuu Mkoa wa Lindi kuwa, katika Halmashauri ya Ruangwa kuna Ugonjwa usio wa kawaida.
Wagonjwa hao, ni kutoka Kituo cha Afya Mbekenyera, ambapo Ndani ya siku 3 (tarehe 5 na 7 Julai 2022), walipokea Wagonjwa 2 katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu (puani), kichwa kuuma na mwili kuchoka sana.
Dkt. Sichwale amesema, Wizara iliunda timu ya wataalam kutoka idara ya Magonjwa ya dharura na Majanga, Epidemiolojia, Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Utafiti (NIMR), Chuo kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na Hospitali ya Taifa Muhimbili, waliungana na timu ya Mkoa ikihusisha pia Idara ya Mifungo.
Hadi kufikia Julai 12, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 13, kati yao, 3 wamefariki.
Wagonjwa wawili, waliokuwa wametengwa katika kituo cha Afya Mbekenyera, wamepona na kuruhisiwa kurudi majumbani mwao, wengine 5 wamejitenga katika makazi yao ya muda kwenye kitongoji cha Naungo, Kata ya Nanjilinji Wilayani Kilwa.
Mgonjwa mmoja ambaye amepona, anaendelea kufanya shughuli zake kijijini Mbekenyera na vile vile watu waliotangamana na wagonjwa hao wamekuwa wakifuatiliwa afya zao kila siku na hadi sasa hakuna aliyeonesha dalili zozote zinazofanana na za wagonjwa hao wakati timu inaendelea na ufuatiliaji.
Ameongeza kuwa, sampuli za awali zilizopimwa katika maabara ya Taifa zimeonesha majibu hasi kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na UVIKO-19.
“Tunaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu pia tunasubiri matokeo ya vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya Binadamu, Wanyama na Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema Dkt. Sichwale.
Amesema, serikali inaendelea kufanya yafuatayo, Kuendelea kutafuta watu wengine wenye dalili kama hizi ili kutambua mapema na kuwatenga ili kuzuia ugonjwa usisambae.
“Kuwatambua watu wote waliotangamana (Contacts) na wagonjwa, wahisiwa, marehemu na kuwafuatilia kwa siku 21,”
“Kutoa matibabu kwa wagonjwa waliobainika kuwa na dalili pia kuwashauri wajitenge wakati wakisubiria majibu ya vipimo vya maabara,”
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii kwa kutumia vyombo mabalimbali vya habari
“Yamefanyika Maandalizi ya dawa, vifaa tiba na vifaa vya kujikinga na maambukizi kwa ajili ya kuwahudumia waathirika endapo watajitokeza tena,”
Hata hivyo, Mganga Mkuu Dkt. Sichwale amesema uchunguzi ukikamilika Wizara itatoa taarifa kwa umma.
Kufuatia harus hiyo, Wizara imetoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati ikiendelea kulifanyika kazi suala hili.
Aidha, imewataka Wananchi waendelee kutumia Vituo vya kutolea huduma za afya pale wanapojisikia kuumwa.