Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia kiasi cha shilingi bilioni 216 kukamilisha mradi umeme kutoka Makambako hadi Songea ikiwa ni moja ya miradi ya kimkakati yenye lengo ya kufanikisha sera ya Tanzania ya viwanda.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ambapo amesema kuwa ifikapo mwisho wa mwezi Septemba mitambo ya mradi huo itawashwa na wananchi wa mikoa ya Njombe na Ruvuma wataanza kufurahia umeme wa uhakika kutoka gridi ya Taifa.
“Mradi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwani wataunganishiwa umeme kwa bei nafuu ya mradi wa REA ambayo ni elfu 27 tu na kuwanufaisha wateja 22,700 hali itakayo wawezesha wananchi kutumia umeme huo kwa ujenzi wa viwanda na shughuli za maendeleo katika maeneo yao” Amesema Dkt. Kalemani
Aidha, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaokoa fedha kiasi cha Shilingi bilioni 9.1 ambazo zinatumika kununua mafuta mazito yanayotumika kwenye mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Madaba, Ludewa, Mbinga, Namtumbo na Songea Mjini.
Hata hivyo, ameongeza kuwa ujenzi wa mradi huo uliotekelezwa na Serikali ya Tanznaia kwa kushirikiana na Serikali ya Sweden umetekelezwa kwa awamu mbili.
Sehemu ya kwanza ya mradi huo imehusisha ujenzi wa vituo vitatu vya kupooza na kusambaza umeme mkubwa wa msongo wa KV 220 vilivyojengwa Makambako, Madaba na Songea na sehemu ya pili ilihusisha ujenzi wa miundo mbinu ya kusafirisha umeme.