Agizo la Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan la watumishi wenye sifa kupandishwa madaraja alilolitoa siku ya kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi Mei Mosi, 2021 limeanza kutekelezwa.
Akizungumza jijini Mwanza leo Jumatatu Juni 14, 2021, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema tayari walimu 1,135 wa Mkoa wa Mwanza wamepandishwa madaraja kutekeleza agizo la Rais Samia.
“Huyo ndiye Rais Samia Suluhu Hassan akiahidi anatekeleza,” amesema Waziri Mwalimu akishangiliwa na wananchi eneo la Mkuyuni jijini Mwanza.
Waziri Mwalimu aliyepewa fursa ya kuzungumzia masuala yanayohusu Wizara yake wakati wa ziara ya Rais Samia ya siku tatu inayoendelea mkoani Mwanza, amesema watumishi wote wenye sifa wataendelea kupandishwa madaraja kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za ajira.
“Hapa Mwanza walimu wanafanya kazi kwa furaha na hamasa kubwa baada ya kupandishwa madaraja, tutaendelea kufanya hivyo kwa kada zote kuhakikisha watumishi wanapata haki na kuongeza ari kazini,” amesema Mwalimu.
Akihutubia kilele cha Mei Mosi mwaka huu, Rais Samia pamoja na mambo mengine aliahidi kuwa Serikali itawapandisha madaraja na kuwalipa stahiki zao watumishi wote wenye sifa.