Serikali imewasilisha Bungeni makadirio ya Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2021/2022 huku ikianisha maeneo ya vipaumbele kwa Mwaka huo wa Fedha.
Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 36.33.
Akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa, kati ya fedha hizo mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.03 sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote.
Amesema kati ya mapato hayo mapato ya kodi ni shilingi trilioni 22.18, sawa na asilimia 13.5 ya pato la Taifa.
Aidha Waziri huyo wa Fedha na Mipango amesema kuwa, Serikali inalenga kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya shilingi trilioni 2.99 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri shilingi bilioni 863.9.
Kwa mujibu wa Dkt. Nchemba, Washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu yenye jumla ya shilingi trilioni 2.96, sawa na asilimia 8.1 ya bajeti yote, kiasi kinachojumuisha fedha za miradi ya maendeleo shilingi trilioni 2.67 na mifuko ya pamoja ya kisekta shilingi bilioni 282.3.
Amewashukuru Washirika wa maendeleo kwa kuendelea kutoa fedha za misaada na mikopo nafuu, ili kufanikisha miradi na programu mbalimbali za maendeleo zitakazotekelezwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022.
Dkt. Nchemba amewataja washirika hao wa maendeleo kuwa ni pamoja na Serikali za Canada, China, Denmark, Finland, India, Ireland, Italia, Korea Kusini, Japan, Ufaransa, Ujerumani, Norway, Poland, Ubelgiji, Uholanzi, Uswisi, Uingereza, Sweden na Marekani.