Tanzania imewataka Mabalozi, Makaimu Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuzingatia sheria za nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao nchini kwa ufanisi na ufasaha.
Akiongea katika mkutano na Mabalozi, Makaimu Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema kuwa mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine yanajengwa katika misingi ya mkataba wa Vienna, Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria mbalimbali, hivyo ni vizuri mabalozi kuzingatia taratibu hizo.
“Sisi kama tumesisitiza kuwa ni vyema mabalozi na wawakilishi wa nchi zao wakafuata taratibu, mila pamoja na desturi zilizopo katika mikataba hiyo ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na kufuatana na mkataba wa Vienna, mkataba wa umoja wa mataifa lakini pia kunga, mila na desturi za kibalozi,” amesema Prof. Kabudi.
Aidha, Waziri Kabudi aliongeza kuwa Tanzania kupitia mkutano huo imeanza ukurasa mpya wa mahusiano na uendeshaji wa shughuli za Serikali na balozi pamoja na mashirika ya kimataifa yaliyopo Tanzania.
“Tunepata nguvu mpya baada ya mabalozi wote kueleza kuridhika kwao kwa hali ya juu sana na hatua ambazo Serikali ya Tanzania imechukua kupambana na rushwa, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, hatua ambazo Tanzania imechukua katika kuimarisha makusanyo ya kodi lakini pia kusimamia matumizi ya fedha za ndani pamoja na zile zinazotolewa na nchi mbalimbali katika maendeleo ya Tanzania,” Amesema Prof. Kabudi.
Katika mkutano huo, Waziri Kabudi amewahamasisha mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kuhusu kuhamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa kuwaeleza maendeleo yaliyofikiwa kuhusu ujenzi wa miundombinu mbalimbali muhimu na kwamba wakati umefika wa kuharakisha kuhamia Dodoma kwa wakati muafaka kwa kuwa maendeleo yaliyofikiwa nayatoa fursa ya kuwawezesha wao kuhamia jijini Dodoma.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mabalozi hao hapa Nchini ambae pia ni Balozi wa Comoro Dkt. Ahamada Mohamed ameipongeza Tanzania kwa kuitisha mkutano huo mapema ikiwa ni siku tisa tu tangu kuanza kwa mwaka mpya wa 2020 kwa nia ya kubadilishana mawazo na kusikiliza changamoto za mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa pia kuwaelezea hatua za utekelezaji za masuala ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli jambo linalowapa fursa mabalozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi hapa nchini.
Nae balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu ambaye pia Kiongozi wa Mabalozi wa Bara la Afrika amesema wao kama mabalozi hawawezi kujua mipango, vipaumbele na changamoto za serikali bila ya kuelezwa na kutaka mikutano ya namna hiyo kufanyika mara kwa mara jambo ambalo linatoa uelewa na muelekeo wa utendaji kazi wa serikali na hivyo kusaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kwa kutambua fursa na changamoto zilizopo…
Awali akiwakaribisha mabalozi katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, aliwataka mabalozi kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu na kanuni za nchi ili kuhakikisha shughuli zao ndani ya Tanzania zinaendana na kufuatana na mkataba wa umoja wa mataifa.
“Nawasihi sana tufanye kazi kwa kuzingatia taratibu za nchi pamoja na sheria na mikataba kwa manufaa ya nchi yetu (Tanzania) na nchi zenu ili tuweze kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina yetu kwa maendeleo endelevu” Amesema Dkt. Mnyepe
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Dkt. Damas Ndumbaro,Katibu Mkuu Dkt Faraji Mnyepe na Mkuu wa Itifaki Balozi, Kanali Wilbert Ibuge, mabalozi 28, Makaimu Mabalozi 12 na Wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa 10.