Aliyekuwa Mshambuliaji wa Azam FC Shaban Chilunda amejipanga kurejea kivingine msimu ujao baada ya kupona majeraha yake.
Chilunda alikuwa anasumbuliwa na majeraha ya goti, ambayo yalimfanya akae nje ya uwanja kwa takribani miezi sita sasa.
Chilunda amesema alipomaliza mkataba wake na Azam FC alipata ofa kutoka nje ya nchi, lakini alipoumia goti hakuwa na namna zaidi ya kujiuguza awe fiti.
“Nakumbuka nilishapata viza na tiketi, kila kitu, lakini nikajitonesha goti, kwahiyo safari nikaona nisiondoke kwa sababu niliumia na nisingeweza kuondoka wakati nina majeraha.
“Nilikwenda Afrika Kusini kujitibia na hii tangu mwaka jana (Desemba), lakini kwa sasa niko fiti namshukuru Mungu na nipo tayari kwa ajili ya msimu mpya,” amesema mchezaji huyo.
Ameongeza kuwa msimu ujao anatarajia kurejea akiwa na nguvu za kutosha kuhakikisha anaendelea kupambania kipaji chake kama ilivyo siku zote.
“Niko fiti kwa asilimia zote na mashabiki watarajie kuniona uwanjani msimu ujao, kuhusu nitacheza wapi inawezekana ikawa hapa hapa ndani au nje,” amesema
Chilunda ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa kwenye kiwango kizuri kwenye kikosi cha Azam FC na baadae aliondoka kwenda Hispania katika klabu ya CD Tenerife, lakini baadaye alirejea Azam FC.