Lydia mollel – Morogoro.
Uongozi wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, umekanusha madai ya Wananchi wanaoishi eneo la Mazoka ambao walilalamika kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii wakidai kunyanyaswa na Mwekezaji wa Africa Agrofocus Tanzania LTD, ukisema taarifa hizo si za kweli ispokuwa walivamia shamba la Mwekezaji huyo.
Eneo hilo la Mazoka, linakadiriwa kuwa na wakazi wasiozidi 1000 ambao wanaendesha maisha yao kwa ufugaji, ambao kwa nyakati tofauti walipaza vilio vyao kwa Serikali wakidai kuharibiwa makazi yao na mwekezaji huyo ikiwemo kuwaleta vikwazo Watoto kufikia huduma za elimu.
Kufuatia malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka alifika eneo la tukio na katika ufafanuzi wake alisema wananchi hao hawaishi kihalali mahala hapo na ujenzi wa makazi yao ya kudumu uliilazimu Serikali kuzungumza na mwekezaji huyo ambaye alikubali kutoa sehemu ya shamba lake ekari 3,000 kwa wananchi hao, ili kuepusha migogoro.
Amesema, mpaka sasa hakuna Mwananchi ambaye ameharibiwa makazi yake, mali wala Mifugo, huku akikemea kitendo cha baadhi ya watu kuwatumia Wananchi hao kwa maslahi yao binafsi.
Kwa upande wake Mwekezaji toka Africa Agrofocus Tanzania LTD, Muzamil Karamagi ameelezea jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika kulinda shamba hilo lisiendelee kuharibiwa na mifugo, ikiwemo kutoa ekari 3000 kwa wananchi hao pamoja na kuwasogezea huduma muhimu za kijamii.