Takriban watu 52 wamekufa na wengine zaidi ya 50 wamejeruhiwa Nchini Pakistan, kufuatia shambulio la bomu la kujitoa mhanga.
Shambulio hilo, limetokea hii leo Sepmtemba 29, 2023 wakati wa sherehe za Kidini huko Mastung Mkoa wa Kusini Magharibi wa Baluchistan, wakati waumini wa Kiislamu wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad.
Akihojiwa na Vyombo vya Habari, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa eneo hilo Munir Ahmed amesema l mshambuliaji alijilipua karibu na gari la Naibu Msimamizi wa jeshi la Polisi, lililokuwa limeegesha karibu na Msikiti uliobomoka na kuwafukia chini ya vifusi watu wengine kati ya 30 na 40.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na mlipuko huo, ambao unajiri huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya makundi ya wapiganaji magharibi mwa Pakistan, hali inayozidisha changamoto kwa Vikosi vya usalama kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Januari 2024.