Wafungwa wa makosa ya kawaida ya jinai wana haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu, baada ya kubatilishwa kwa kifungu cha 11(1) (c) cha Sheria ya Taifa Uchaguzi kinachoweka zuio kwa wafungwa wanaotumikia adhabu ya kunyongwa na wanaotumikia adhabu ya kifungo cha kuanzia miezi sita.
Hayo yamebainishwa na Mahakama kuu nchini kufuatia hukumu iliyotolewa na Jaji Elinaza Luvanda Desemba 22 ikitokana na shauri la Kikatiba lililofunguliwa na raia wawili, Tito Magoti na John Tulla ambao walikosa haki ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 wakati wakiwa mahabusu.
Raia hao, walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masijala Kuu, mwaka huu 2022, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Jeshi la Magereza, wakidai kuwa kifungu hicho kinakinzana na Katiba Ibara ya 5(1) ambayo inaeleza kuwa kila raia wa Tanzania kwenye umri wa miaka 18 anayo haki ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wakipinga madai hayo, walidai kuwa NEC imekuwa ikiwawezesha raia wote kutekeleza haki hiyo kwa mujibu wa sheria, huku Jaji Luvanda katika uamuzi wake akikubaliana na hoja za Wakili Seka kwa niaba ya wadaiwa kuwa zuio hilo kwa wafungwa wote wanaotumikia adhabu kuanzia miezi sita kinakiuka Ibara ya 5(1) ya Katiba.