Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda amesema kuwa atatolea ufafanuzi kuhusu  hatima ya mvutano uliopo kati ya Vyama vya Siasa na Serikali kuhusu mikutano ya hadhara ndani ya siku 21 zijazo.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni takribani mwezi mmoja baada ya kuchaguliwa  na baraza hilo kuwa mwenyekiti akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray.

Amesema tangu Serikali ya awamu ya Tano iingie madarakani hali ya kisiasa imekuwa na mvutano mkubwa na hali hiyo imekuwa ikisababisha kutokea sintofahamu miongoni mwa wanasiasa.

“Sisi kama Baraza tunahitaji vyama vya siasa  na wanasiasa kufanya siasa za maendeleo na si za kulumbana, kwani hazina tija kwenye maslahi ya nchi,”amesema Shibuda.

Aidha, Shibuda amevitaka vyama vya siasa kufikisha madai yao kwenye baraza hilo ili liweze kuchukua hatua stahiki na kuachana na utaratibu wa kila chama kuzungumza lake.

Hata hivyo Shibuda amesema kauli za baadhi ya viongozi  wa vyama vya kisiasa zinaweza kuwa sababu ya Serikali kufanya uamuzi ambao unalalalmikiwa hivyo kuwataka wasome alama za nyakati.

 

David Abdallah Burhan Afariki Dunia
Video: Waliofukiwa siku 3 mgodini wasimulia, Maalim Seif: Nitakuwa Rais Z'bar