Katika hali ya kustaajabisha, wanafunzi na mabinti kati ya miaka 10 hadi 15 katika mkoa wa Shinyanga wamekuwa wakipelekwa na wazazi wao kwa waganga ili kuogeshwa dawa za kuvutia wanaume maarufu kama ‘samba’.
Jambo hilo limepelekea shirika lisilo la kiserikali la Kivulini kuomba serikali kuingilia kati na kupiga marufuku tabia hiyo kwa kuwa inachochea maambukizi ya virusi vya Ukimwi na mimba za utotoni.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kivulini linalojihusisha kupinga ukatili kwa watoto na wanawake, Yassin Ally amesema vitendo hivyo vinakwenda kinyume na mikakati ya Serikali ya kutokomeza Ukimwi na mimba za Utotoni.
Amesema vitendo hivyo vinafanyika kwa wingi mkoa wa shinyanga na kufafanua hivi karibuni alikwenda kutoa semina kwa baadhi ya shule na kuelezwa wanafunzi wa kike wamekuwa wakikosa masomo kutokana na kwenda kuogeshwa.
“Wiki iliyopita nilikwenda mkoa wa Shinyanga, nilifika baadhi ya shule na kukuta wasichana wenye umri kati wa mika 10 hadi 15 ni watoro, nilipodadisi sababu ya kushindwa kufika niliambiwa wanakwenda kuogeshwa dawa za mvuto maarufu samba” Amesema Ally
Na kuongeza ” chaajabu walimu wanajua kabisa, watendaji wa vijiji, vitongoji na hata waratibu elimu wanafahamu lakini wanashindwa kuchukua hatua ili kukomesha”.
” Wito wangu Serikali kupitia kwa wakuu wa mikoa, makamanda wa polisi, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapige marufuku vitendo hivyo na wafuatilie kwa ukaribu na kuwachukulia hatua wazazi” amesisitiza Ally.
Amesema vitendo hivyo kama vikiendelea kuachwa bila kuwekewa adhabu kali, itakuwa kazi ngumu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake ambao mwishowe huishia kwenye maradhi kama Ukimwi, mimba za utotoni na utelekezaji familia.